FAHAMU SANA .......
Add caption
JARIBU KUSOMA UJITAMBUE WEWE NI NANI
Kuna msichana mmoja aliona maisha magumu mno, kila alichokifanya alikiona kushindikana jambo lililomkatisha tamaa. Kila alipokuwa akilitatua tatizo hili, kuna tatizo jingine liliinuka na kumfanya kuchanganyikiwa.
Hakutaka kuendelea kuishi maisha ya namna hiyo, alichoamua kukifanya ni kumfuata mama yake na kisha kumuelezea matatizo aliyokuwa akikutana nayo. Sauti yake tu, ilisikika kama mtu aliyekuwa amekata tamaa na kutokata kuendelea na maisha yale.
Mama yake hakusema kitu, alichokifanya ni kumchukua na kumpeleka jikoni. Akachukua maji na kuyaweka jikoni, yalipocheka, akachukua karoti akaziingiza katika maji yale, akachukua mayai na kuyaingiza katika maji yale na mwisho kuchukua kahawa na kisha kuiingiza katika maji yale bila kusema kitu chochote kile.
Kila kitu kilipochemka, akayatoa mayai yale na kisha kutoa karoti zile katika maji yale na kisha kumuuliza 'UMEONA NINI?'
"Nimeona karoti, mayai na kahawa," alijibu.
Mama yule akamtaka binti yake aziguse karoti zile, binti alipozigusa, akagundua kwamba karoti zimekuwa laini sana. Hakuishia hapo, akamtaka ayachukue mayai yale na kuyavunja.
Yule binti alipoyavunja, akagundua kwamba yamekuwa magumu tofauti na kipindi kile, kabla ya kuyaingiza ndani ya maji yale yaliyokuwa yamechemka.
Mwanamke yule hakuishia hapo, akamwambia aonje maji yale yaliyokuwa yamechanganywa kahawa, alipoyaonja, akayahisi yamebadilika ladha na kuwa matamu sana.
"Una maana gani kufanya haya yote mama?" msichana yule alimuuliza mama yake aliyeanza kumjibu hivi:
"Kabla sijaweka karoti ndani ya maji, zilikuwa ngumu sana ila baada ya kuziweka ndani ya maji yanayochemka, zikabadilika na kuwa laini sana. Sikuishia hapo, nilichokifanya ni kuyachukua mayai na kisha kuyaweka ndani ya maji yanayochemka, kilichotokea, mayai yale yaliyokuwa laini, yakabadilika na kuwa magumu.
"Nilipoweka kahawa ndani ya maji, matokeo yake kahawa ile ikabadilisha maji yote. Kumbuka kwamba vitu hivyo vitatu vimepitia katika kitu kimoja, maji yaliyokuwa yakichemka. Hebu niambie binti yangu, wewe ni nani? Karoti, yai au kahawa?"
CHA KUJIFUNZA
Wote tunapitia katika matatizo mbalimbali. Hatutakiwi kuwa karoti kwamba tunapopitia humo tunakuwa laini na mwisho kukata tamaa, wote tunatakiwa kuwa kama yai, tunaingia humo kwenye matatizo tukiwa legevu lakini mara tunapoyashinda tunakomaa na kuwa wenye nguvu na wagumu. Ila pamoja na hayo yote, katika kipindi ambacho tunapitia katika matatizo mbalimbali yatupasa kuwa kahawa zaidi, kwa kupitia matatizo yetu basi marafiki zetu wote wanaotuzunguka waweze kubadilika kupitia sisi na hata wakati mwingine kuwabadilisha wale ambao wametufanya sisi kuingia katika matatizo hayo.
HEBU KUWA MUWAZI, UNAPOINGIA KWENYE MATATIZO WEWE HUWA NANI? KAHAWA, YAI AU KAROTI?

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii